Timu ya Taifa ya Tanzania chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) inaendelea na maandalizi kwa ajili ya Fainali za mataifa Afrika (AFCON) zinazotarajiwa kufanyika Aprili mwaka huu.Timu hiyo iliyopo kambini Kituo cha Ufundi cha TFF Mnyanjani, Tanga imecheza mechi mbili za kirafiki hadi sasa ikiwa ni sehemu ya kujipima huku ikiwa na matarajio ya kupata mechi nyingine zaidi kama sehemu ya maandalizi.Katika maandalizi yake chini ya Kocha Elieneza Nsanganzelu , kikosi hicho kinaendelea kuboreshwa kabla ya kwenda kwenye Fainali hizo.Pia Kocha Elieneza alisema timu yake iliyopo Karatu mkoani Atusha kwa ajili ya ziara ya mechi za kirafiki inatarajia kurejea Mnyanjani, Januari 30, 2026 baada ya kukamilisha mechi yake ya tatu ya kirafiki. “Tulirejea kambini tarehe 18 Januari kwa ajili ya mazoezi ya kawaida ya kila siku, ikiwa pia ni sehemu ya maandalizi ya Fainali za AFCON.“Tumejumuisha wachezaji ambao wapo kwenye uangalizi baada ya kupita kwenye majaribio (scouting) kwenye maeneo mbalimbali nchini.“Licha ya kukaa kwa muda mrefu kambini vijana hawa bado kuna umuhimu wa kupata mechi nyingi zaidi za kimataifa za kirafiki. Hilo ndilo zaidi kwa sasa TFF inafanyia kazi,” alisema Elieneza.Alisema kuna haja kwa Serikali na wadau mbalimbali kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika maandalizi ya timu hizo ikiwemo ya U15 inayojiandaa na ASFC 2026 hasa katika kupata mechi nyingi zaidi za Kimataifa za kirafiki.

