Timu ya Taifa ya Wanawake U20 (Tanzanite) inayotarajia kushuka dimbani ugenini dhidi ya Kenya, Februari 7, 2026 imedhamiria kufunga hesabu zote kwenye mechi hiyo.

    Tanzanite iliyokuwa kambini kwa takribani wiki mbili chini ya Kocha Bakari Shime imethibitisha kuwa imejiandaa vyema kuikabili Kenya ili kujiweka kwenye mazingira salama zaidi ya kusaka tiketi ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Poland baadae mwaka huu.

    Akizungumzia maandalizi, Kocha Msaidizi Edna Lema alisema wamejiandaa vyema huku wakiiendea mechi hiyo kwa lengo la kuhakikisha wanapata ushindi kabla ya kucheza mechi ya marudiano.

    “Kufahamiana kwetu na Kenya ndio kutasababisha mchezo mgumu, lakini vilevile utakuwa mzuri kwa timu zote.

    “Kikubwa tumewaandaa wachezaji wetu kimwili na kiakili tayari kwenda kuwakabili wapinzani, tunataka tushinde mchezo wa ugeni ili tusiwe na kazi kubwa nyumbani,” alisema Edna.

    Kwa upande wa nahodha wa timu hiyo Jamila Rajabu alisema wachezaji wapo tayari na wote wana ari ya kupata nafasi ya kuipambania Tanzania.

    Amewataka Watanzania wawe na imani ya kutosha juu yao, sambamba na kuahidi ushindi kwenye mechi hiyo.

    Tanzanite itacheza mechi ya marudiano dhidi ya Kenya Februari 14, 2026 katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

    Share.