Mechi za Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) zimeendelea January 13, 2026, kwa mzunguko wa nane huku timu zikiendelea kuonesha ushindani mkubwa ili kujikita kwenye nafasi za juu katika msimamo wa ligi hiyo.
Mechi zote zilipigwa saa 10 jioni ambapo Ceassia Queens walifanikiwa kumvuta shati Mashujaa Queens kwa mechi yao kumalizika kwa suluhu, matokeo yaliyodhihirisha ugumu na uimara wa safu za ulinzi za timu zote hizo.
Bunda Queens wakiwa nyumbani katika Uwanja wa Karume, Musoma walifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Geita Queens.
Katika mechi nyingine ya kuvutia, Simba Queens ikiwa mwenyeji iliiadhibu Tausi FC mabao 3-0 katika Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Mambo yameendelea kuwa mazuri kwa Alliance Girls baada ya kubakiza pointi nyingine tatu kwenye uwanja wao wa nyumbani wakiwalaza Bilo FC bao 1-0.
Wakicheza nyumbani Fountain Gate Princess walizitema pointi zote tatu baada ya kulala mabao 5-4 mbele ya Yanga Princess. Hiyo ilikuwa mechi iliyoongoza kwa kutoa mabao mengi katika mzunguko huo.
Mechi nyingine za ligi hiyo zinatarajia kuchezwa Januari 18 ambao utakuwa ni mzunguko wa tisa.

