Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) imepangiwa kundi B Fainali za Kombe la Afrika kwa Wanawake (WAFCON) zinazotarajiwa kufanyika kuanzia mwishoni mwa Machi nchini Morocco.

    Twiga itaungana na timu nyingine tatu kwenye kundi hilo ikiwemo Afrika Kusini ambao wana kumbukumbu ya kutoka nao sare kwenye WAFCON ya 2024.

    Timu nyingine zinazokamilisha kundi hilo ni Burkina Faso na Ivory Coast.

    Akizungumzia hatua hiyo, Kocha Mkuu wa Twiga, Bakari Shime alisema benchi lake la ufundi limeendelea kufanya kazi kwa ukaribu na wachezaji ili kuhakikisha kikosi chake kinakuwa tayari kabla ya Fainali hizo.

    “Licha ya umbali wa namba kubwa ya wachezaji wetu, tunawasiliana nao kwa karibu na kufanyia kazi makosa madogo madogo wakiwa kwenye klabu zao.

    “Tumepanga kuitumia vizuri Kalenda ya FIFA katika kuandaa timu yetu ili kuhakikisha tunafikia malengo yetu,” alisema Kocha Shime

    Alisema malengo yao makubwa ni kuhakikisha timu inafika nusu fainali na kuwa miongoni mwa timu nne zitakazocheza Kombe la Dunia.

    Twiga Stars inatarajia kutupa karata yake ya kwanza Machi 17 dhidi ya Afrika Kusini, kisha Burkina Faso Machi 20 na kumalizana na Ivory Coast kwenye hatua ya makundi Machi 23.

    Share.